Friday 16 January 2015

RIP Makame Mzee Suleiman



Friday, 16 January 2015

CCM ZANZIBAR YAOMBOLEZA KIFO CHA MWASISI WA ASP MAREHEMU MAKAME MZEE SULEIMAN

Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamepokea kwa mshituko, huzuni na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha aliyewakuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar marehemu Makame Mzee Suleiman, kilichotokea usiku wa tarehe  16 Januari, 2015, nyumbani kwake Amani, Unguja.

Marehemu Makame Mzee Suleiman, alizaliwa tarehe 14 Aprili, 1926, katika Kijiji cha Mitakawani, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini, Unguja.

Alipata Elimu ya Msingi katika Skuli ya  Uzini mwaka 1936. Aidha, alijiendeleza na Masomo ya Qur’an katika Kijiji hicho cha Mitakawani. Mwaka 1945, marehemu alijiendeleza na Elimu ya Sekondari.

Mbali ya Elimu ya Sekondari aliyoipata marehemu, pia alipata mafunzo mbali mbali ndani na nje ya nchi yetu.

Marehemu Makame Mzee, alijiunga na Chama Cha Afro Shirazi (ASP) mwaka 1957 na ni miongoni mwa Waasisi wa Chama Cha Mapinduzi mwaka 1977, katika Tawi la Mitakawani.

Katika uhai wake, marehemu aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali ndani ya Chama na Serikalini. Kwa upande wa Chama na kutokana na uhodari, uwezo na weledi mkubwa wa masuala ya kisiasa, Chama Cha ASP kilimteua kushika nafasi za uongozi zifuatazo :-

·         Mwaka 1957 - 1961, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa ASP Tawi la Mitakawani.

·         Mwaka 1961 - 1977, aliteuliwa kuwa Katibu wa ASP wa Wilaya ya Kati. Pia alikuwa :

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa ASP Taifa.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya

Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Wilaya

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM wa Wilaya na Mkoa wa Kusini, Unguja.

  

Kwa upande wa Serikali, marehemu alibahatika kushika nyadhifa mbali mbali ikiwa ni pamoja na :

Katibu wa Baraza la Mapinduzi (1964 - 1972).

Mkuu wa Wilaya ya Kati, Unguja mwaka 1972 - 1974.

Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Pemba mwaka 1974 - 1978.

Mshauri wa Rais wa Mambo ya Siasa - 1978.

Kwa kutambua mchango wake mkubwa katika Uongozi na Utumishi wa Umma, mwaka 2014, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, alimtunuku marehemu Nishani ya Miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake kinaungana na wanafamilia, ndugu na marafiki wa marehemu na kuwaomba wawe na moyo wa subra katika wakati huu mgumu wa maombolezi ya mpendwa wetu huyo.

Bila ya shaka kifo cha marehemu kimeacha pengo kubwa kwa Taifa letu.

Hadi kufariki kwake, marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman, alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar.

Marehemu ameacha vizuka wawili na watoto ishirini (20).

Tunamuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema Peponi. AMIN.  

 

1 comment:

HKJanuary 16, 2015

Inna Lillahi Wainna Ilayhi Rajiun. Mwenyeez Mungu asameh kwa yote, ampumzishe palipo pema - AMEN.

Pole kwa wote ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo. Hakika kwa kila kiumbe chake Mwenyeez Mungu, basi kifo ndio akhiri yetu.


0 comments:

Post a Comment