Tuesday 27 January 2015

Ushuhuda Huu wa Mzungu Kuhusu Wauza Madawa ya Kulevya

Jan 26, 2015

Ushuhuda Huu wa Mzungu Kuhusu Wauza Madawa ya Kulevya 'Unga’ Ufanyiwe Kazi

Kwa zaidi ya wiki tatu sasa, Watanzania wamekuwa wenyeji wa mgeni ambaye ujio wake nchini umekuwa wa aina yake. Tunaweza kusema ugeni huo siyo wa kawaida, kwani tumezoea kuona ziara za wanasiasa, wafanyabiashara na wageni wengine wengi kutoka katika mataifa mbalimbali wanaokuja kwa ziara za kiserikali na nyinginezo, mbali na watalii wanaotembelea nchi yetu kujionea vivutio lukuki vilivyosambaa kila sehemu.

Hata hivyo, ziara ya Padri John Wootherspoon, raia wa Australia aliyekuja nchini Januari Mosi, mwaka huu ni tofauti kabisa na ziara nyingine tulizozizoea. Yeye anaishi China na amepata kibali cha Serikali ya China kutembelea magereza mbalimbali nchini humo na kuwafariji wafungwa. Katika kufanya kazi yake hiyo katika magereza nchini China na majimbo yake ya Hong Kong na Macau, amekutana na wafungwa wengi kutoka nchi mbalimbali duniani na kugundua kwamba kilichowaingiza magerezani ni biashara ya dawa za kulevya.

Kabla ya kuja hapa nchini, Padri Wootherspoon aliliambia gazeti hili, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likifuatilia huduma zake katika magereza nchini China kuwa, alikuwa na mpango wa kuitembelea Tanzania baada ya kugundua kwamba idadi ya Watanzania wanaotumikia vifungo katika magereza mbalimbali nchini China ni kubwa mno ikilinganishwa na wafungwa wengine kutoka nchi nyingine. Anasema wafungwa zaidi ya 130 kutoka Tanzania wako katika magereza ya Shek Pik, Stanley, Loo Woo na Macau na kwamba kila mwezi Watanzania wanne hadi sita wanafungwa magerezani kwa makosa hayo.

Kutokana na hali hiyo, Padri Wootherspoon aliamua kuja Tanzania kwa gharama zake mwenyewe ili kuwasaidia wafungwa hao kuwasiliana na familia zao hapa nchini, baada ya kupata mawasiliano ya familia hizo kutoka kwa wafungwa hao. Anasema wafungwa hao walitumiwa tu na wafanyabiashara wakubwa (ambao majina yao tunayahifadhi kwa sasa) kupeleka dawa hizo nchini China na kwamba tangu awasili nchini amewasiliana na familia nyingi za wafungwa hao, ambazo amesema zimo katika umaskini mkubwa. Padri huyo tayari amekutana na Kamishna wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, ACP Godfrey Nzowa na kumtaka aende nchini China kupata taarifa za kina kutoka kwa wafungwa hao.

Sisi tunadhani ziara ya Padri huyo hapa nchini ni fursa ya pekee kwa Serikali kupata taarifa muhimu za kusaidia kutokomeza biashara hiyo. Juni, mwaka jana Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi alisema wakati wa kuadhimisha Siku ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya Duniani kwamba kazi ya kuwanasa vinara wa biashara hiyo imekuwa ngumu na akisema vijana wa Kitanzania 65 kati ya 403 waliokamatwa nchi za nje kwa kuhusika na usafirishaji wa dawa za kulevya wamehukumiwa kunyongwa nchini China.

Waziri Lukuvi pia alisema vitendo vya rushwa vimekwamisha jitihada na mikakati ya kuwatia mbaroni vigogo wa biashara hiyo. Bahati nzuri ni kwamba Padri Wootherspoon yuko nchini kama sehemu ya suluhisho la tatizo hilo.

Ni matarajio yetu kwamba Serikali itafanya kila linalowezekana kushirikiana naye ili kupata taarifa muhimu zitakazosaidia kuwakamata wamiliki wa biashara hiyo. Hatua hiyo pia itaondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa wananchi kwamba kikwazo kikuu katika vita ya kukomesha uhalifu huo kimo ndani ya Serikali yenyewe.

0 comments:

Post a Comment